Previous Lesson -- Next Lesson
1. Utakaso wa maisha yako hupatikana kwa kujitoa kabisa kwake Mungu (Warumi 12:1-2)
WARUMI 12:1
"1 Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.“
Watu wa agano la kwanza walithibitisha shukrani zao kwa wema wa Mungu kwa njia ya matoleo mbalimbali hekaluni. Walitoa dhabihu, kwa alama ya kujitoa wenyewe, na sadaka za wanyama kwa kila kosa lililojulikana, na kwa kufanya hivyo waliondoa dhambi zao mbele za Mungu. Baada ya kuharibiwa kwa hekalu kule Yerusalemu, Paulo aliwashauri hao waumini ndani ya Kristo, waliokuwa watu wa lile agano la kwanza na kuishi Rumi kwamba, wasitoe fedha au sadaka kwa Mungu. Badala yake wajitoe wenyewe na miili yao na hivyo kujikabidhi kabisa kwake Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kujitoa namna hii kuonyeshe kwamba, hao si mali yao wenyewe tena, bali sasa ni mali ya Mungu kabisa.
Jambo hilo latuongoza moja kwa moja kwa swali linalopasa kuulizwa na kila Mkristo: „Je, wewe bado ni mali yako mwenyewe, au umejitoa kama sadaka kwake Mungu kwa thibitisho la kuokolewa na Kristo?
Sadaka hiyo haimaanishi kwamba, inawapasa Wakristo wajitoe wenyewe kufa, bali wafanye juu chini wasilegee tena na waanze kumtumikia Mungu kwa kutumia roho na akili zao, mwili, fedha, na vitu vyote walivyo navyo. Sadaka hiyo inajumlisha na mapambano ya kiroho dhidi ya majaribu yote ya miili yetu, maana miili yetu inatamani kinyume cha roho, na roho zetu kinyume cha mwili. (Wagalatia 5:17). Paulo anajitaja mwenyewe kuwa mfano wa mstari huo: „Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu“ (Wagalatia 2:20).
Mtume Paulo alijifungamanisha mwenyewe kabisa na kwa milele na Kristo kwa kiasi kwamba, alijihesabia kuwa amekufa, na kuishi kipekee kwa uhai wa Kristo aliyopewa na Roho Mtakatifu. Kwa maana iyo hiyo mtume anakuuliza wewe utoe maisha yako kwake Mungu na Mwana wake, ili upate kuwa mtu mwenye haki. Kristo atakutakasa kwa njia ya damu yake na kwa kuishi kwa Roho yake ndani ya mwili wako, ili upate kuwa sadaka takatifu inayokubalika na Mungu. Zawadi hizo mbili, yaani damu ya Kristo na kutawala kwa Roho yake ndani yako,ndiyo uzima wa milele utakayopewa. Kwa hiyo, rudi kwa Baba yako wa mbinguni na kwa rehema yake isiyo na mwisho, ili aweze kukujaza kwa upya na nguvu yake takatifu kila siku.
Mtume Paulo anarejea kwa hatua ya kujitoa kikamilifu kwa Mkristo kama ndiyo: „ibada yenu yenye maana“ (Warumi 12:1). Kuimba kwako kwa furaha ni jambo la msingi katika ibada yako kwake Mungu, na sala zako na maombezi zina nguvu sana, lakini Bwana naye anatazamia uamuzi wako wa mwisho kujitoa mwenyewe kabisa kwake kwa daima na milele. Hii ndiyo hali ya kujifunga kiinjili, ambayo inatendeka mara moja tu. Ila ndipo agano hilo jipya linaingia maishani mwako, na uzima wa milele pia inaingia maishani mwako.
SALA: Ee Baba wa mbinguni, tunakuabudu na kushangilia, kwa sababu kutokana na malipo ya Kristo wewe umepata kuwa Baba yetu mwenye rehema. Tusaidie tusiendelee kuwa na umimi na ya kunang‘ania, bali kutoa muda wetu, uwezo wetu, na nafsi zetu kwa mwana wako, na tufaulu kukataa dhambi na uchafu. Tia upendo wako ndani yetu, ili tupate kuishi ndani ya namna ya wema wako tele: Amina.
SWALI:
- Je, umejitoa kabisa mwenyewe kwa daima kwake Yesu, Mwokozi wako, au bado unaendelea na hali ya umimi na kuishi kwa ajili yako tu?