Previous Lesson -- Next Lesson
WARUMI - BWANA NDIYE HAKI au UADILIFU WETU
Masomo kuhusu Barua ya Paulo kwa Warumi
SEHEMU 3 - HAKI YA MUNGU HUJIONYESHA MAISHANI MWA WAFUASI WA KRISTOS (Warumi 12:1 - 15:13)
1. Utakaso wa maisha yako hupatikana kwa kujitoa kabisa kwake Mungu (Warumi 12:1-2)
WARUMI 12:2
"2 Wala msiifuatishe namna ya dunia hii, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.“
Paulo hakuwatazamia washiriki wa kanisa la Rumi wapuuze ile roho na ukweli wa umoja wa Utatu Utakatifu; kwa hiyo aliwaita waingie kwenye vita ya kiroho dhidi ya aina zote za majaribu ya kutenda dhambi.
Gombano hilo la kiroho halimfikishi mtu pa kupokea wokovu, maana tayari Kristo amekuokoa, ila Bwana wako anatazamia haki yake ipate kuonekana kwa njia ya utakaso wa maisha yako.
Sasa Paulo anatolea njia zinazoweza kufanyika kwa ajili ya utakaso wa maisha yako:
a) Kwamba kuanzia sasa hutaishi kwa wasiwasi kama wale wanavyofanya bila Kristo, au kutafuta heshima, ustaarabu, ashiki au kujifurahisha kwa namna mbalimbali, lakini kupokea tabia takatifu ya maisha ya Yesu na jinsi walivyoishi mitume yake; hayo yawe mawazoni na kwenye utendaji wa maisha.
b) Kwa kuishi kufuatana na miongozo hii, Bwana atakujalia kufanya upya tabia zako. Lengo lako lisishikamane na mwenendo wa ustaarabu, bali ufikirie mawazo ya Mungu, ili roho ya neema iweze kutakasa moyo wako na hali ya kutaka kwako.
c) Heri utambue mapenzi ya Mungu, pia na ufahamu Mungu anayoyataka kwako, ili uweze kutenda kufuatana na makusudi yake, na kukataa yale anayokataa yeye. Ili ufikie hali hii ya kukomaa kiroho, lazima usome Biblia takatifu kwa kurudia, na hivyo kutafuta uongozi, mwelekeo na hali ya kumulikiwa na Baba yako wa mbinguni, ili uweze kumpendeza na kumridhisha kamili.
d) Paulo alisema kwa urahisi: Fanya mema. Usiseme tu habari ya mema, bali utende, ukitoa yote mawili, muda wako na fedha zako. Jifunza kwake Mungu yaliyo mema na yaliyo mabaya, na utofautishe vizuri kati ya hayo mawili maishani mwako. Jipatie hekima toka kwa Biblia takatifu, ndipo Roho Mtakatifu atakufundisha kufikia yote yale yanayompendeza Mungu.
e) Tafuta hali ile ya kukamilika kiroho maishani mwako. Sharti hiyo haimaanishi kwamba, utaweza kujikamilisha wewe mwenyewe. Kwa hiyo, umwulize Yesu akujazie mapungufu yako, ili yote utakayotenda kwa ajili yake yawe kamili, na yenyewe, na ya kweli. Hayo yataweza kutendeka ndani yako kama zawadi ya umoja wa Roho Mtakatifu, ikiwa utayatafuta kwa bidii.
f) Kama utaishi kwa namna hii, utaishi na Mungu, na ndipo Roho wa Mungu atatenda kazi ndani ya mapungufu yako nawe utapata kuwa mtu wa furaha, ukimshukuru Mungu kwa ajili ya sadaka yake ya kujitoa mwenyewe kule Golgotha.
SALA: Ee Baba wa mbinguni, utusamehe hapo tulipokuwa na hali ya kujifikiria wenyewe tu, wa kujipenda wenyewe zaidi ya wewe. Ubadilishe makusudi yetu, ili tuishi kwenye huduma ya kweli kiroho; hali tumetambua na kukumbuka kwamba, Yesu ametusamehe dhambi zetu zote kule msalabani, na Roho yako Mtakatifu amepata kuwa nguvu ndani ya maisha yetu. Utusaidie, ee Bwana, tupende kabisa kujitoa kabisa kwako kwa siku zote mbeleni.
SWALI:
- Zipi ndizo hatua za kuishi maisha matakatifu kwa wafuasi wa Yesu?