Previous Lesson -- Next Lesson
3. Watu wote ni wapotovu na wenye hatia ( Warumi 3:9-20)
WARUMI 3:9-10
"9 Ni nini basi? Tu bora kuliko wengine? La! Hata kidogo. Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wayunani ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi; 10 kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja .“
Paulo akajumlisha lalamiko lake dhidi ya wote Wayahudi na wa Mataifa katika jina la Mungu, akawahakikishia wote kwamba, hakuna aliye na upendeleo au mafao mbele za wengine. Wote wametenda dhambi, na dhambi zao ni dhahiri. Wametoka kwenye njia ya Mungu iliyonyoka, na wakawa watumwa wa dhambi, hali wamefungwa na tamaa na kujidanganya wenyewe. Paulo alijijumlisha pamoja ndani ya malalamiko hayo, akikiri kwamba, yeye naye alikuwa mwenye dhambi.
Je, umewahi kuona wakati wowote jambo fulani lililokuwa la kuchukiza sana kwamba, ukapata kutapika? Makosa yako ni ya kuchukiza mno kwamba, yanafanya roho na moyo wako zitapike. Ujilinganishe mwenyewe na malalamiko ya Paulo, nawe utatambua kwamba, ni wewe mwenyewe unayeelezwa mle.
WARUMI 3:11-12
"11 Hakuna afahamuye; hakuna amtafutaye Mungu. 12 Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja
Sisi sote tu wachafu mbele za utukufu wa Mungu unaon’gaa kabisa. Hakuna aliye mwenye haki ila Kristo. Akili zetu zimezungukwa na mvuke mnene, nasi hatuwezi kumwona Mungu, aliye mwimo wetu mkuu, jinsi alivyo Yeye. Hatutambui dhambi zetu zilivyo za kuchukiza kabisa. Heri watu wangekuwa na bidii ya kutafuta utukufu wa Mungu, ili wakapate kuwa wenye akili! Basi tu, kila mmoja achukua njia yake mwenyewe, akishikana na heshima yake mwenyewe, hali amefungwa na tamaa yake, akitafuta tu raha. Watu wote wamepotelewa na njia ya Bwana wao, na hakuna atembeaye katika njia iliyo ya kweli. Wewe sio bora katika tabia yako hata kidogo. Wote wamekwenda upande, wakawa watu wasioleta faida na wanakwenda kupotea. Sisi sote tu wapotovu tangu asili, na dhamiri yetu inatujua kikamilifu.
WARUMI 3:13
"13 Koo lao ni kaburi wazi, kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira i chini ya midomo yao.”
Uchafu wa watu hujionyesha kwenye ndimi zao. Sote tu wauaji na wachinjaji, kwa sababu tunaleta uharibifu na maangamizi ya heshima, furaha na amani ya wengine kwa njia ya ndimi zetu kali; tunatia sumu kwenye tabia kwa maongo, mashtaka, matukano na maneno ya kuchekesha bila haya; pia tunalalamika dhidi ya miongozo ya Mungu. Upinzani wetu ni kama unajisi chungu midomoni mwetu. Sisi ni wenye kutokutii nidhamu ya Mungu, na hatutambui kwamba, hatustahili lolote ila mapigo mazito na hukumu ya lazima.
WARUMI 3:14-17
"14 Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu. 15 Miguu yao ina mbio kumwaga damu. 16 Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao. 17 Wala njia ya amani hawakuijua.
Chuki yetu haiwezi kubadilika haraka, maana hatuwataki adui zetu, bali twataka tuondolewe na watu wagumu. Watu wanaowachukia adui zao wanamwaga mito ya damu, kwa sababu mwanadamu katika hasira yake hugeuka kuwa kama mnyama mkali. Hakuna amani ndani yetu, mbali na porojo zetu nyingi kuhusu amani. Watu wote ni wauaji tu, na mioyo yao imejaa na dharau, ukorofi na kiburi, kwa sababu hawajui kwamba, Mungu ni upendo, kweli na usafi. Walipoteza akili kuhusu ukweli, wala hawana taratibu au utulivu, lakini walijidondosha wenyewe katika hali ya hatari.
WARUMI 3:18
"18 Kumcha Mungu hakupo machoni pao.”
Hao wote wasiomjua Mungu ni wapumbavu; na wote hao wasiomcha yeye wamepungukiwa na hekima, kwa sababu kicho cha Bwana ndiyo mwanzo wa hekima, na kumfahamu Aliye Mtakatifu ndiyo ufahamu wa kweli. Hali ya kutokuamini inazidi kukua siku hizi, na watu wanajiweka kana kwamba hakuna Mungu. Basi, si ajabu kwa sababu hiyo, dhambi imezidi mno, na inainua kichwa chake kwa ushupavu barabarani, ndani ya magazeti na pia mioyoni mwa watu!
WARUMI 3:19-20
"19 Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu; 20 kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.“
Watu wa Mungu wakati wa Agano la Kale wote pia ni watenda dhambi, kwa sababu sheria iliwawezesha kutambua dhambi. Ni kweli kwamba, sheria inatuahidi pamoja na baraka zote za mbinguni, ikiwa tutashika maagizo yote ya sheria, lakini hakuna mtu awezaye kutimiza sharti hii. Wakati wowote tunapojitahidi kujijenga kwa bidii yetu sisi wenyewe, mahusiano yetu maovu hutokea ndani ya damu yetu. Sisi sote tunastahili tu adhabu ya Mungu, na matendo yetu mema yote yamechafuka na choyo yetu, wala hatuwezi kumpendeza Mungu. Je, unakubaliana na miongozo hiyo ya Paulo? Rudia tena kusoma yale aliyoyaandika, ili upate kuwa mwenye busara na kuvunjika mbele za Bwana.
SALA: Ee Baba wa mbinguni, tunakushukuru kwa sababu ulitujalia tumaini ndani ya Kristo kwamba, tunaweza kufikia hali ya kutokukata tamaa wala kuona yote ya maisha kuwa mabaya. Wote tu wabaya mioyoni mwetu, kwenye ndimi zetu, mikononi, miguuni na machoni; na mioyo yetu imejaa udanganyifu, chuki, tamaa mbaya na maongo. Loo, jinsi nilivyo mtu mchafu sana! Nisamehe dhambi zangu, na uchore utakatifu wako mbele za macho yangu, ili na vipande vyote vya kiburi vivunjwe ndani yangu, nami nipate kukuabudu wewe tu katika ukweli. Ee Bwana niondolee kabisa na dhambi zangu zote. Amina.
SWALI:
- Jinsi gani Mtume alibainisha (weka wazi) dhambi zetu, akizilinganisha na upotovu wa binadamu wote?
QUIZ - 1
Mpendwa Msomaji,
Baada ya kusoma maelezo yetu ya Barua ya Paulo kwa Warumi kwenye kitabu hiki (au kwenye internet), utakuwa unaweza kujibu maswali yafuatayo. Ukifaulu kujibu 90% (tisini kwa mia) ya maswali hayo hapo chini, sisi tutakutumia sehemu ifuatayo ya mfululizo huo, yakusaidie kwa maongozo yako mema. Tafadhali usisahau kutaja jina lako nzima na anwani yako waziwazi kwenye karatasi ya majibu yako.
- Zipi ni kusudi na mwisho wa Barua kwa Warumi?
- Ni nani aliyeanzisha Kanisa la Rumi?
- Nani aliyeiandika barua hii? Na wapi? Na lini?
- Paulo alitumia mitindo gani katika kuiandika barua hii?
- Ipi ni mpangilio wa barua hii?
- Ipi ni vyeo, ambavyo Paulo alivichukua kwa ajili yake mwenyewe, vilivyo kwenye sentenso ya kwanza ya barua yake?
- Nini ni maana ya tamko kwamba, Kristo ni Mwana wa Mungu?
- Neema ni nini, na jibu lake mtu liwe nini kwa neema hiyo?
- Tamko gani ndani ya Mbaraka wa Kitume unahesabu kuwa lenye uzito zaidi na na kukufaa wewe zaidi kuhusu maisha yako?
- Kwa nini Paulo alikuwa akimshukuru Mungu kila wakati?
- Jinsi gani, na mara ngapi Mungu alimzuia Paulo kutimiza mipango yake ya binafsi?
- Tamko gani ndani ya mstari wa 16 unafikiria kuwa muhimu zaidi? Na kwa nini?
- Jinsi gani haki ya Mungu inahusika na imani yetu?
- Kwa nini ghadhabu (au Hasira) ya Mungu imefunuliwa?
- Kwa nini inampasa mtu aishiye bila Mungu ajitengenezee mungu wa kidunia kwa ajili yake mwenyewe?
- Yapi ni matokeo ya kutokumwabudu Mungu ilivyo sawa?
- Jinsi gani Paulo alifafanua jambo la kutokea kwa ghadhabu ya Mungu?
- Taja dhambi zile tano katika orodha ya madhambi, ambazo unahisi ni zile zinazoenea zaidi katika ulimwengu wetu wa siku hizi?
- Jinsi gani mtu anajipatiliza mwenyewe anapomhukumu mwingine kwa jambo lolote?
- Zipi ni zile siri, ambazo Paulo anatufunulia kuhusu hukumu ya Mungu?
- Jinsi gani Mungu atawashughulikia watu wa Mataifa katika Siku ya Hukumu?
- Zipi ni kanuni tukufu zitakazotumika katika hukumu ya mwisho?
- Zipi ni mapendeleo na pia mizigo ya sheria (torati) juu ya Wayahudi?
- Maana ya kutahiriwa ni nini katika zote mbili Agano la Kale na Agano Jipya?
- Yapi ni maswali ya kimsingi yaliyopingana katika barua ya Paulo kwa Warumi, na yapi ni majibu yake?
- Jinsi gani Mtume alibainisha (weka wazi) dhambi zetu kwa kulinganisha na upotovu wa binadamu wote?
Ukikamilisha kujifunza vitabu vyote (au masomo yote) ya mfululizo huo juu ya Warumi na kutuma kwetu majibu yako kwa maswali mwishoni mwa kila kitabu, tutakutumia:
CHETI CHA
masomo ya kuendelea katika kufahamu barua ya paulo kwa Warumi
ili utiwe moyo kwa ajili ya huduma yako kwa Kristo hapo mbeleni.
Tunataka kukutia moyo ukamilishe na mitihani kuhusu Barua ya Paulo kwa Warumi, ili upate hazina ya kudumu. Tunangojea majibu yako na tunakuombea. Anwani yetu ni hii:
Waters of Life
P.O.Box 600 513
70305 Stuttgart
Germany
Internet: www.waters-of-life.net
Internet: www.waters-of-life.org
e-mail: info@waters-of-life.net