Previous Lesson -- Next Lesson
a) Tambulisho na Mbaraka wa kitume (Warumi 1:1-7)
WARUMI 1:5-7
“5 ambaye katika yeye tulipokea neema na utume, ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake; 6 ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo; 7 kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu.”
Yesu Kristo ndiye ufunguo kwa vipawa vyote kutoka kwa Mungu. Si manabii wala watakatifu, hata Bikira Mariamu hawawezi kupatanisha kwa ajili yako mbele za Mungu kwa neema au baraka. Baba wa mbinguni hujibu maombi yetu kwa sababu ya Yesu Kristo, maana yeye ndiye wa pekee anayetuombea kwa Mungu. Jina lake ni kama mfereji, ambayo ndani yake sala zetu zinapitishwa kwake Mungu, na kwa njia hiyo vipawa vyote vya kiroho hutufikia. Hakuna mwingine ila Yesu aliyetupatanisha na Mwenye Utakatifu. Hivyo, twapokea toka kwake ukamilifu wa neema inayojumlisha msamaha, amani, wokovu na haki. Mibaraka mingine tukufu nazo ni kama nyongeza, ambazo hatuzistahili hata hivyo.
“Neema” ndiyo jumlisho la barua ya Paulo. Yeye aliona jambo hilo vema ndani ya nafsi yake, maana alikuwa ni mtesi wa kanisa. Aliokolewa si kwa sababu ya juhudi zake, sala au matendo mema, lakini kwa sababu ya rehema ya Mungu aliyemjalia ndani ya Kristo. – Hivyo basi, peleka kwa yeyote habari njema ya neema kuu na ya kikamilifu, jinsi Kristo alivyokupatia wewe kwanza neema, msamaha na amani.
Basi, mara utakapofahamu na kukiri taratibu ya neema, wewe utakuwa ni mbebaji wa neema, mhubiri wa upendo wa Mungu, na mjumbe wa usuluhisho wa bure. Je, Roho Mtakatifu aliweka ujumbe wake moyoni mwako? Au bado uko kimya, mwenye huzuni, na kufungwa na kamba za dhambi zako?
Yeyote atakayetambua ujumbe wa neema, yeye atampenda Mungu na Kristo wake, naye atatii amri zake za wema wake. Neno hilo “utii kwa ajili ya imani” kwake Paulo ina maana ya itiko la mtu kwa ajili ya neema hiyo. Mungu hakudai kwetu utii kinyume cha mapenzi yetu kwa ukorofi au kutokuridhika kwetu, bali kujitoa kabisa kwa mioyo yetu iliyokombolewa katik shukrani kwa Mwokozi na Msuluhisha wetu. Paulo alijiita mwenyewe kuwa ni mtumwa wa Yesu Kristo. Kwa cheo hiki alitoa mfano kamili kwa neno hilo “utii kwa ajili ya imani”. Je, wewe ni mtumwa wa Kristo? Mungu aliwasamehe watu wote, tena wakati wowote, pia na dhambi zote kwa ajili ya Kristo. - Kwa sababu hatuoni ujumbe mwingine wa kufaa na wa kusaidia watu kuliko ujumbe huo, basi tunawakaribisha wote tunaowafahamu wajitoe kwa Mungu na kumpenda Kristo wake, na hivyo watambue nguvu ya neema yake.. Loo, jinsi ujumbe huu ulivyo kuu! Je, uliwahi kuwaita rafiki zako watii imani ndani ya Mtoaji wa neema yote?
Washiriki wa kanisa la Rumi walikuwa wameitwa moja kwa moja na Kristo, wala si na Paulo au mtu yeyote mwingine. Hii ndiyo siri ya imani sahihi: kwamba hakuna mtu amwitaye mtu mwingine kwenye wokovu, isipokuwa huyu aitaye yu katika hali bora kabisa, maana tu vyombo mkononi mwa Bwana wetu. Yesu huwachagua na kuwaita wafuasi wake binafsi na kwa wazi. Sauti yake inadidimia hadi kwenye kina cha chini mioyoni, maana ni sauti yake Yule afufuaye wafu. Neno „Kanisa“ linamaanisha ushirikiano wa waalioitwa, waliowaacha wale waonao yote kuwa mabaya, na waliopokea wajibu wa upendo katika kumtumikia Mungu. - Je, wewe ni mwitwa wa Yesu Kristo? Au upande mwingine, wewe bado hufai na kuwa bila matunda? Dini yetu ndiyo dini wa kuitwa.
Yeyote anayekubali na kujibu wito huo, yeye ni mpendwa wa Mungu. Jinsi ilivyo nzuri sana na yenye utukufu lile tamko linaloeleza wazi Wakristo ni watu wa namna gani! Wao ni jamaa wa Aliye Juu, nao wanajulikana kwake na kuheshimiwa naye. Zaidi ya hapo, Mungu alishuka kwenye daraja lao, na kwa sababu ya kafara yake, aliwafanya wastahili ushirikiano wake. Upendo wa Mungu ni kubwa zaidi na safi mno kuliko upendo wa wazazi kwa watoto wao, au hata kati ya bibi na bwana arusi. Upendo wa Mungu ni takatifu wala hauwezi kukosa kabisa. – Je, wewe ni mmojawao wa wapendwa wa Mungu, na kujaa na upendo wake, pia na kutembea katika utakatifu wake?
Kristo alituita kwa maisha ya msamaha, utii na ufuasi. Na kilele cha sifa hizi ni utakatifu. Hakuna aliye mtakatifu ndani yake au kwa bidii yake, lakini kwa njia ya utumishi wetu pamoja na Mwokozi wa kutukomboa tumepata kustahili kwa kumpokea Roho Mtakatifu. Kwa njia ya neema tu twaweza kuwa takatifu na bila lawama mbele za Mungu katika upendo.
Watakatifu wote wamejitenga na dunia na wameamriwa kwa huduma ya Mungu. Wao si mali yao wenyewe tena, wala si wa jamaa zao, kwa sababu wamepata kuwa mali ya Mungu kwa ajili ya kazi ya utakatifu. - Je, wewe ni mmojawao? Wewe kweli ni takatifu kwa neema?
SALA: Mungu wetu mtakatifu, wewe ulituita katika Yesu Kristo tupate kuwa takatifu, jinsi ulivyo takatifu. Tunakiri kutokufaa kwetu na tunaomba msamaha kwa ajili ya dhambi zetu zote tunazozijua na kutokuzijua. Twakushukuru kwa sababu unatupenda na kutusafisha na damu ya Kristo, na kututakasa kwa njia ya Roho wako Mtakatifu. Badilisha maisha yetu yote, ili tuwe wako kwa nguvu zetu zote na muda wote, na tukupende wewe jinsi unavyotupenda sisi.
SWALI:
- Neema ni nini, na jibu lake mtu liwe nini kwa neema hiyo?