Previous Lesson -- Next Lesson
d) Pilato aliogofya kwa hali tukufu ya Kristo (Yohana 19:6-11)
Yohana 19:8-11
„Basi Pilato aliposikia neno hilo, akazidi kuogopa. Akaingia tena ndani ya Praitoria, akamwambia Yesu, Wewe umetokapi? Lakini Yesu hakumpa jibu lolote. Basi Pilato akamwambia, Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya kukusulibisha? Yesu akamjibu, Wewe hungkuwa na mamlaka yoyote juu yangu, kama usingpewa kutoka juu; kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.”
Pilato alikuwa na shaka juu ya nafsi yake Yesu. Unyofu wake, usafi na upendo wake hayakuwa bure kwa huyu mtawala. Kwa hiyo alipogundua kwamba Yesu hatajwi tu kuwa mfalme, lakini pia kuwa ni Mwana wa Mungu akatishwa. Warumi na Wayunani walitambua mbinguni kuwa na roho na miungu ambao kwa wakati waweza kuwa na mwili na kutembea kati ya watu. Yeye akitambua hayo akafikiri, “Je, pengine huyu ni mungu aliyechukua hali ya mwanadamu?” Basi akamwuliza, “Umetoka wapi?”
Yesu hakutumia nafasi hii ya kutoroka kuadhibiwa, bali akanyamaza. Ukimya huo ulikuwa wa kuonya. Mungu hajibu maswali kuhusu mawazo ya kiakili tu, au ya udadisi, bali hujifunua kwake aaminiye na kutegemea ndani yake. Huwa anatofautiana kabisa na maoni ya kiyunani au kirumi juu yake, maana hakuna afananaye naye. Kwa ukimya huo, Pilato akachukia na kuuliza, “Je, hutaki kusema nami? Ninayo uwezo kuua au kukuruhusu; wewe u chini ya enzi yangu. Adui zako wanadai kusulibishwa kwako. Mimi pekee naweza kukuokoa au kukutundika.” Basi Yesu akaitika, “Kweli unaweza. Baba yangu alikupatia mamlaka hiyo. Wewe huna uwezo ndani yako mwenyewe. Ubatili wako utajionyesha hivi karibuni katika tamko la hukumu isiyo haki. Baba yangu wa mbinguni anayo uwezo wote, na mimi pia. Hakuna mamlaka duniani, isipokuwa kwa kibali chake.” Kibali hicho mara nyingi itajionyesha katika uharibifu, jinsi ilivyotokea kwa Pilato, aliyejaliwa enzi kwa ruhusa tukufu. Mungu atawala historia yote, ila aruhusu watu washiriki katika kuwajibika kwa ajili ya matendo yao. - Wewe nawe unawajibika kwa namna unavyowatendea na wengine.
Yesu alimwambia Pilato, “Umekosa sana, lakini si wewe tu uliye kosa. Wote wameshikwa ndani ya nyavu za dhambi. Wewe hutaki kunisulibisha, lakini woga wako na hofu kwa ajili ya Kayafa zinakufanya uniadhibishe.” Kuhani Mkuu alikuwa na hatia kubwa zaidi, maana alitaka kumsulibisha Yesu kwa sababu ya wivu na chuki. Kwa vile alishika ofisi kuu, angetakiwa kuonyesha huruma kwa ajili ya wenye kosa kubwa, ili kuwapatanisha na Mungu. Lakini yeye alikuwa amepagawa na roho mbaya, alimchukia Yesu kiasi cha kutaka kumwua.
e) Pilato kutamka hukumu bila haki juu ya Yesu ( Yohana 19 : 12-16 )
Yohana 19:12
“Na tangu hapo Pilato akatafuta kumfungua; lakini Wayahudi wakapiga makelele wakisema, Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kasari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari.”
Pilato alitamani kumfungua Yesu, maana mfungwa huyu alimthibitishia enzi yake. Mbali na mamlaka yake Kristo, utukufu wake uliweka mipaka kwa enzi hiyo. Yesu hakumtisha Pilato, ila kumkemea kwa upole. Tena akafanya utofauti kati ya kosa la Pilato na tendo la kuvunja sheria la Kayafa. Kwa hali halisi Yesu ndiye aliyekuwa hakimu wake aliyemhoji, naye akajaribu kumvuta upande wa hali halisi wa Mungu.
Makuhani wa kiyahudi walipotambua mabadiliko katika msimamo wa moyo wa Pilato, wakabadilisha hojiano kwenye siasa. Mashitaka yao kwamba Yesu alidai utakatifu haikufaa kwenye baraza la Kirumi. Hivyo wakamtisha mtawala kumwonyesha kutokuwa mwaminifu kwa Kaisari, asipomwua Yesu.
“Kuwa rafiki wa Kaisari” ilimaanisha kupendelewa na Mtawala Mkuu. Jina hilo la heshima walijaliwa wajumbe wake na wa ukoo wake wa utawala. Pengine mke wa Pilato alikuwa mmojawapo mwenye uhusiano huo. Kwa vile Kaisari Tiberio hakumwamini yeyote, pia kuwa na hali ya asili ya kuona yote kuwa mabaya, alielekea kuwa na mashaka juu ya uaminifu wa wajumbe wake. Daima alitazamia machafuko yanayoongozwa na mmojawapo. Yeyote aliyeweza kumshitaki rafiki fulani wa Kaisari na kuthibitisha shitaka lake, basi aliweza kumwangusha huyu mstakiwa hadi kufukuzwa kabisa.
Kama viongozi wa Kiyahudi wangalituma barua Rumi kwamba, Pilato “alimwachilia huru Mfalme wa Wayahudi”, tena pamoja na mashitaka yao kuwa ni mwenye fujo, ingemaanisha kwamba anakusanya maadui wa Kaisari kumzungukia. Kwa sababu hiyo utawala wake Pilato ilitikiswa. Hakuwa tayari kunyakuliwa huo utawala wake kwa ajili ya Yesu, iwapo ukweli ulikuwa upande wake Yesu. Basi tisho hilo ilivunja hali yake ngumu dhidi ya Wayahudi na akatayarisha kutamka sentenso kumhukumu Yesu. Akarudi nyuma kwenye mambo ya ofisi yake ya kujilinda nafsi yake na damu ya Kristo. Kwa nje alionekana kwamba alipitisha hukumu ya haki, lakini kwa undani wa moyo wake alifahamu kwamba hakutumia haki kabisa.
Yohana 19:13-16a
“Basi Pilato, aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti chake cha hukumu, mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha. Nayo ilikuwa Maandalio ya Pasaka, yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi, Tazama, Mfalme wenu! Basi wale wakapiga kelele, Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Je, nimsulibishe mfalme wenu! Wakuu wa makuhani wakamjibu, Sisi hatuna mfalme ila Kaisari. Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe …”
Pilato alikuwa akidharau tumaini la Wayahudi la kumtazamia Masihi, akadhihaki maneno yao ya kuasi Rumi na kusema, “Mmemshitaki Yesu aliyedai ufalme! Chukueni ufalme wenu usio na mamlaka! Mnafanana na huyu, hamstahili hata kujaliwa nami!” Wayahudi wakaelewa kiini cha dharau hilo, ikageuza malalamiko yao dhidi ya Yesu kwenye dharau la washitaki wake. Wakalia kwa sauti moja, “Mpeleke msalabani, yeye ni aibu, amelaaniwa! Msulibishe!”
Ndugu, hao waliopiga kelele walijifikiria kuwa na haki kufuatana na sheria zao, lakini walikuwa wamepofuka, bila kuweza kutambua upendo ulioingia mwilini na kwa wema wake kwa ajili ya wadogo, wala utakatifu wa Mungu uliotimia ndani ya Yesu hawakuiona. Walimchukia na kuhitaji tu kumwondoa kabisa. Si ushupavu wala bidii itawavuta watu kwa Mungu; upendo tu ulivyoonekana ndani ya Yesu utaweza kufumbua macho yetu kwa rehema zake na kwa sadaka aliyoileta.
Pilato alielekeza dharau lake kwa Wayahudi waliochafuka, na tena akamwita Yesu kuwa “Mfalme”, na hivyo kufunua thibitisho kwamba wote waliohudhuria walikusudia kumwua Yesu. Pilato alijaribu kupata singizio kwa dhamiri yake iliyomshitaki kwa ndani, lakini umati wa waliaji waliunganika katika shabaha yao ya kumsulibisha Yesu. Sauti ya watu kwa vyovyote sio sauti ya Mungu, maana mara nyingi wanakosa katika tamaa zao na msukumo wa kidunia, naye Shetani anatumia makosa yao kwa makusudi yake.
Makuhani walikuwa na uchungu kwa ajili ya dharau ya Pilato tena na tena. Wakaunganika tena kwa kutamka la kushangaza, “Hatuna mfalme ila Kaisari.” Tamko hilo ndani yake ilikuwa ni unafiki. Ukoo wa kikuhani walihofia mwamko wa ki-masihi, pamoja na kumchukia Herode mfalme wa kubandia. Walimwona afadhali Kaisari kama mlinzi wa ustaarabu wa Kiyunani pamoja na sheria na taratibu nchini. Lakini hivyo waliasi utabiri wa Agano la Kale na tumaini lote la ki-masihi. – Baba wa uongo huwadanganya moyoni watoto wake. - Hata hivyo Yesu pekee alisimama barazani katika ukweli, akisikiliza sauti ya Mungu katika dhamiri yake na kushikamana kabisa na uaminifu wake.
Mwishoni Pilato akapitisha maamuzi hayo makali, akiongozwa na ubinafsi wake, ukorofi na udanganyifu. Mwana wa Mungu akaendelea kuwa kimya, akitegemea uongozi wa Babaye, aliyemruhusu mtawala kumsulibisha Mwana wake. Kwa hukumu hiyo isiyokuwa na haki, Yesu alikamilisha upatanisho kati ya Mungu na binadamu. WaleRoho wa kishetani walidhania kwamba wamefaulu, lakini ilikuwa ni mipango ya Mungu yaliyotimilika hapo, kinyume cha shauri la hila la majeshi ya kuzimu.
Sala: Bwana Yesu, tunakuinamia; wewe ndiwe Mwana Kondoo wa Mungu, ucchukuaye dhambi za ulimwengu mzima. Utujalie moyo wa rehema, wenye uaminifu na unyofu. Utusaidie tusitumie wengine kwa ajili ya faida yetu, na utuwezeshe kuona bora kufa kuliko kukubali udanganyifu au kupatana na maovu.
Swali 114: Kwa nini Pilato alitamka hukumu juu ya Yesu ?