Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- Romans - 081 (Greetings from Paul’s fellow Workers)
This page in: -- Afrikaans -- Arabic -- Armenian -- Azeri -- Bengali -- Bulgarian -- Cebuano -- Chinese -- English -- French -- Georgian -- Greek? -- Hausa -- Hebrew -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Malayalam -- Polish -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish? -- Tamil -- Telugu -- Turkish -- Urdu? -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

WARUMI - BWANA NDIYE HAKI au UADILIFU WETU
Masomo kuhusu Barua ya Paulo kwa Warumi
Maongezo kwa SEHEMU ya 3 - Maelezo ya pekee juu ya msimamo wa Paulo kwa viongozi wa kanisa la Rumi (Warumi 15:14 – 16:27)

7. Salamu kutoka kwa watenda kazi pamoja na Paulo (Warumi 16:21-24)


WARUMI 16:21-24
"21 Timotheo, mtenda kazi pamoja nami, awasalimu, na Lukio, na Yasoni, na Sosipatro, jamaa zangu. 22 Mimi Tertio, niliyeandika waraka huu, nawasalimu katika Bwana. 23 Gayo, mwenyeji wangu, na wa kanisa lote pia, awasalimu. Erasto, wakili wa mji, na Kwarto, ndugu yetu, wanawasalimu. 24 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi nyote. Amina."

Ni kwa mara chache tu twamwona Paulo peke yake. Kila wakati huwa anazungukwa na watenda kazi wake na washiriki wazoefu katika utume wa Bwana, kama vile Barnaba na Sila, kwa ajili ya kumsahihisha, kwa kumshauri, pia na kumwangalia kwa usalama wake. Mara kwa mara waumini wengine kutoka kwa miji kadhaa walishiriki katika mwenendo wa ushindi wa Kristo, ambayo Paulo alijikuta kuwa mtumwa aliyeandamana kwa shangilio, hali amefungwa gari la ukuu wake; kana kwamba alilazimika kufukiza uvumba kwa ajili ya ukuu wake Kristo, na yeyote aliyevuta huo uvumba angeokoka, bali kila aukatae angeangamia (Warumi 2:14-16).

Paulo aliandika waraka wake kwa Warumi katika mwaka wa Bwana 59, wakati alipotulia mjini Korintho, ambapo wafuasi wa Kristo kadha wa kadha walishiriki naye, nao wakaongeza salamu zao mwishoni mwa waraka huu. Salamu hizo zaonyesha kwamba, Paulo hakuandika peke yake, kama vile mwana filosofia, bali alizungukwa na kundi, ambalo lilimshauri kwa vipengele mbalimbali kuhusu waumini wa kule Rumi. Kwa sababu hiyo basi ushirikiano wa watakatifu unaonekana wazi ndani ya waraka wake huu.

Timotheo alikuwa amekulia kwa mkono wa mama yake Mkristo wa kiyahudi, aliyejitoa kabisa kwake Kristo, pia na kwa bibi yake aliyekuwa na sifa ya imani na kuwa mcha Mungu. Baba yake alikuwa ni Myunani, asiyejulikana kinaganaga. Paulo aliona ndani ya mtu huyu mwema, aliyempenda Kristo, mshiriki wa kufaa kwa utume wa Mungu, akiwa na urithi wa kisemiti na kiyahudi ndani yake. Hata hivyo, Paulo alimtahiri, kwa sababu mama yake alikuwa ni Myahudi, kwa kusudi yeye naye apate kuwa Myahudi kamili kwa Wayahudi wengine, pia na Myunani kwa ajili ya Wayunani. Wote wawili walitenda kazi katika ushirikiano kamili, na Timotheo alikuwa kwake Paulo kama mwana.

Timotheo hakutafuta mambo yake mwenyewe, lakini aliishi ili amtukuze Bwana Yesu, naye alitafuta kwanza ufalme wa Mungu na haki yake. Paulo alimtuma mara kwa mara alipokuwa safarini aende kwa miji kadha, ili atayarishe kukaa kwake na kwa huduma yake Paulo pamoja na wajoli wake. Mara nyingine ilimpasa Paulo kumwacha peke yake, kwa sababu ya kufukuzwa kutokana na kudhulumiwa kwake. Timotheo alikuwa anawajibika kwa malezi ya kiroho ya wale waumini wapya (Matendo ya Mitume 16:1-3; 19:22; Wafilipi 2:19-22).

Baada ya salamu zake Timotheo, watu watatu wa kabila la Paulo wanatajwa, kwa majina ni jamaa zake Lukio, Yasoni na Sosipatro. Yasoni ndiye mtu aliyemkaribisha Paulo wakati wa kukaa kwake Thessalonike, wakati wa machafuko yaliyosababishwa na Wayahudi, baada ya hoja ya Paulo nao kwa Masabato matatu, na kwa kufaulu kwa Paulo na Sila kupata watu waliookoka, ambao pamoja nao wakaanzisha kanisa jipya kwa ajili ya Kristo. Ghasia ya watu walishambulia nyumba ya Yasoni, na walipokosa kuwapata Paulo na Sila, wakamburuza Yasoni mbele ya mtawala wa mji na kumshitaki kwamba, anafuata imani mpya, inayomtambua Yesu kuwa Mfalme wa wafalme, anayewazuia watu kuendeleza utii wao kwake Kaisari. Lakini mtawala aliwafukuza Wayahudi wakorofi na kumwachisha Yasoni kwa dhamana (Matendo ya Mitume 17:6).

Sosipatro alikuwa ni mwumini kutoka Beroya, ambapo Wayahudi walipokea neno la Paulo kwa utulivu, pia wakachunguza vitabu vya Agano la Kale siku kwa siku ili wagundue, kama yule Msulibiwa aliyefufuka kutoka kwa wafu kweli ni Masihi. Basi Wayahudi walitengeneza tena fujo, waliposikia habari ya kuhubiri kwake Paulo kule Beroya, ila watu wa Beroya walimsindikiza Paulo kwa heshima aende Athene, lakini Sila na Timotheo walibakia Beroya, ili wawaimarishe waliookoka kiimani na katika kweli kamili. Ndipo tunasoma kwamba, mtu aitwaye Sosipatro alimsindikiza Paulo kwenda Yerusalemu, ili apeleke michango ile ya ukarimu kwa wale wenye haja kule.

Jamaa wa tatu wa Paulo anaaminiwa kuwa ni Lukio wa Kirene (Matendo ya Mitume 13:1), aliyekuwa ni mzee katika kanisa la Antiokia, naye alimsindikiza Paulo kwa sala zake.

Tertio alikuwa ni mtu Mrumi aliyeweza kusema Kiyunani bila shida, na jina lake latajwa mwisho wa waraka huu kwamba ndiye mwandishi au katibu, ambaye Paulo aliandikisha waraka huu kwa Warumi. Paulo aliandikisha kwake neno hadi neno, naye alikuwa na muda wa kutosha kukamilisha kazi hiyo kuu, kwa sababu huyu mwandishi alitumia kwa kazi hiyo kalamu yake kwa kuandika kwenye karatasi ya mafunjo. Huduma hiyo iliendeshwa katika ushirikiano kamili na wa karibu. Ilimpasa Tertio aelewe kabisa maana ya Paulo, ili aweze kuandika yote katika uaminifu kwa kanisa la Rumi. Paulo alimhesabia Tertio kuwa mmojawapo wa wachaguliwa, aliyekuwa na misingi imara ndani ya Bwana Yesu, naye alitayarisha kanisa la Rumi vema, na wao walimfahamu vizuri na kumtegemea.

Gayo alikuwa ni mwumini kutoka Thessalonike, aliyemkaribisha Paulo nyumbani kwake wakati alipofukuzwa, na pia alifungua milango yake kwa ajili ya mikutano ya kanisa. Gayo aliwashughulikia watu kadhaa waliomjia na matatizo yao, naye alikuwa ni mmoja wa wale wachache ambao Paulo aliwabatiza mwenyewe kule Korintho kufuatana na tamko lake: „Nashukuru, kwa sababu sikubatiza mtu kwenu, ila Krispo na Gayo, ….. Maana Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Habari Njema (1.Wakorintho1:14-17).

Erasto alikuwa ni mtunza hazina wa mji aliyehudumia kazi yake kwa uaminifu na sifa. Hayo yaonyesha kwamba, kanisa la Korintho halikuwa na maskini au watu wa kawaida tu, lakini pia na watu wa hali ya juu zaidi, waliokuwa na sauti katika jamii ya mji. Kwarto alikuwa ni ndugu katika Kristo; hakuwa Myunani, bali Mrumi aliyejulikana na kanisa wakati ule.

SALA: Tunakushukuru, Ee Bwana Yesu, kwa sababu unao watumishi ndani ya kanisa lako wanaohudumia kwa moyo wao wote katika huduma mbalimbali za utawala na za kiroho. Twaomba uwasaidie wazee wa makanisa yetu wawe waaminifu katika yote wayatendao kwa utukufu wa jina lako takatifu.

SWALI:

  1. Nani ndiye mtu ambaye Paulo alimwandikisha waraka wake kwa Warumi?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on November 17, 2022, at 01:17 PM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)