Previous Lesson -- Next Lesson
c) Onyo kwa waumini wa toka Mataifa wasiwe na kiburi juu ya watoto wa Yakobo (Waisraeli) (Warumi 11:16-24)
WARUMI 11:16-24
"16 Tena malimbuko yakiwa matakatifu, kadhalika na donge lote; na shina likiwa takatifu, matawi nayo kadhalika. 17 Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa, na wewe mzeituni mwitu ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzabibu na unono wake, 18 usijisifu juu ya matawi yake; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe. 19 Basi utasema, Matawi yale yalikatwa kusudi ili nipandikizwe mimi. 20 Vema. Yalikatwa kwa kutokuamini kwao, na wewe wasimama kwa imani yako. Usijivune, bali uogope. 21 Kwa maana ikiwa Mungu hakuyaachia matawi ya asili, wala hatakuachia wewe. 22 Angalia basi, wema na ukali wa Mungu; kwa wale walioanguka ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, ukikaa katika wema huo; kama sivyo, wewe nawe utakatiliwa mbali. 23 Na hao pia, wasipokaa katika kutokuamini kwao, watapandikizwa; kwa kuwa Mungu aweza kuwapandikiza tena. 24 Kwa maana ikiwa wewe ulikatwa ukatolewa katika mzeituni, ulio mzeituni mwitu kwa asili yake, kisha ukapandikizwa kinyume cha asili, katika mzeituni ulio mwema, si zaidi sana wale walio wa asili kuweza kupandikizwa katika mzeituni wao wenyewe?“
Paulo anahakikisha kwamba, Ibrahimu alihesabiwa haki kwa imani, naye anatambua kwamba, wazaao wa Ibrahimu nao wangehesabiwa haki ikiwa wanaamini alivyoamini baba yao, maana kama mizizi ya mti ilikuwa njema, matawi yake nayo yangepasa kuwa mema; na kama mikate ya kwanza ilikuwa tamu sana, mikate mingine ya donge lile pia lingekuwa tamu sana. Mwanzoni Wakristo nao walikuwa wageni katika ufalme wa Mungu. Walikuwa kama matawi ya mzeituni iliyokuwa jangwani, lakini mkono wa Bwana aliwapandikiza ndani ya mzeituni mwema wa zamani, kama vile Ibrahimu na ukoo wake, ili wao nao wapate kuishi kutokana na haki yake, na pia wabebe matunda kutokana na nguvu yake. Lakini kama mkono wa Bwana ulikata baadhi ya matawi ya asili ili apandikize ndani yake matawi mageni, hayo matawi yaliyopandikizwa haiyapasi kupata kiburi, yakijifikiria yenyewe kuwa bora na yenye thamani zaidi kuliko yale yaliyoondolewa.
Wayahudi basi ni kama yale matawi yaliyoondolewa kwa sababu walimkataa Kristo na kuchukia Wokovu wake, wakati hayo matawi mapya yaliyopandikizwa yanaonekana kuwa Wakristo waliopokea imani katika Mwana wa Mungu. Hao waliopandikizwa kwa upya ni wepesi kujivuna wenyewe, wakisema kwamba, watoto wa Ibrahimu ni wakorofi na wanachukia. Basi yeyote apataye kiburi na kujisifu mwenyewe, mapema ataanguka ndani ya uharibifu. Ndiyo maana Paulo anawaonya waumini hao waliokuwa wa Mataifa, wasije wakajisifu mno.
Mtume anaendelea na kuhakikisha kwamba, Mungu mtakatifu aliye na haki zote hakujuta kwa ajili ya yale matawi ya asili, kwa vile hayakuleta matunda, ingawa alikuwa amesema nao mara nyingi kwa ahadi zake. Angeona bora kuyakata hayo matawi yaliyopandikizwa hivi karibuni, kama yalibeba ugonjwa fulani ndani ya hali yao, na yasingeruhusu nguvu kutokana na zizi la zamani kuwatengeneza. Paulo anasema habari ya wema na ukali wa Mungu wakati fulani. Pia na uaminifu wa Mungu unaonekana katika kazi yake ya kukata matawi yasiyobeba matunda, kama hayatoi nafasi yapate kufanywa upya, kusafishwa na kutakaswa. Wema wa Mungu unatambulikana ndani ya wale wanaopata kupandikizwa katika Kristo, maana yeye ndiye mzeituni wa kiroho, nao watatengenezwa na kuzaa sana wakisimama imara ndani yake; lakini wakipata kuwa wapumbavu na kuzuia kazi ya Roho Mtakatifu, yeye atawakata tena kabisa.
Yesu alikuwa ameeleza taratibu hiyo aliposema: „Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea“ (Yohana 15:5-6).
Hata hivyo Myahudi, aliyewahi kuwa tawi aliyeondolewa kutoka katika mzeituni wa zamani, na pia amekubali sasa kuamini ndani ya Yesu na uungu wake na kupokea utakaso wake, atapandikizwa tena kwa mkono wa Bwana. Mungu aweza kutenda hayo ya ajabu. Anaweza kutia tena uhai ndani ya matawi yaliyokatwa, na kwa sababu hiyo baadhi ya Wayahudi wanaweza kurudi kwenye imani kwa Mwokozi wao Yesu.
Kwa ajili yetu basi, Mungu hakutuchukia wakati tulipokuwa bado watenda dhambi; bali sasa alitutakasa wakati wa ungamo wetu kwa njia ya damu ya Kristo. Naye alituhuisha kwa njia ya Roho wake Mtakatifu. Kwa taratibu hiyo anakusudia kuwaokoa watoto wote wa Ibrahimu, pia pamoja na kabila la Ismaeli, pia na watoto wa Yakobo, ikiwa nao watatafuta ukweli. Yesu huwapandikiza ndani ya shina, ili watoe matunda mengi ndani ya kila mmojawao.
SALA: Ee Baba wa mbinguni, tunakushukuru kwa sababu umetusafisha sisi wanadamu tusio na adabu, ukatutakasa kwa neema yako, na ukatupandikiza ndani ya mwili wa kiroho wa Kristo. Jinsi upendeleo huu ulivyo mkuu sana uliotujalia sisi bure! Tunashangaa. Basi tusaidie tusiishi kwa ajili yetu sisi tu, au kupata kiburi, bali tujibidiishe kuwaingiza wengi wa wale wasio na adabu wafikie maisha yako yaliyo bora.
SWALI:
- Kupandikizwa ndani ya mwili wa kiroho wa Kristo inamaanisha nini?
- Nani atakuwa hatarini, kama kule kupandikizwa kutaharibika?