Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- The Ten Commandments -- 04 -- Second Commandment: Do Not Make Idols
This page in: -- Afrikaans -- Arabic -- Armenian -- Azeri -- Baoule -- Bengali -- Bulgarian -- Cebuano -- Chinese -- English -- Farsi -- Finnish? -- French -- German -- Gujarati -- Hebrew -- Hindi -- Hungarian? -- Indonesian -- KISWAHILI -- Malayalam? -- Norwegian -- Polish -- Russian -- Serbian -- Spanish -- Tamil -- Turkish -- Twi -- Ukrainian? -- Urdu? -- Uzbek -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

TOPIC 6: AMRI KUMI - Kuta za ulinzi wa Mungu zinazolinda wanadamu wasianguke
An Exposition of the Ten Commandments in Exodus 20 in the Light of the Gospel

04 - Amri ya Pili: Usijifanyie Sanamu



KUTOKA 20:4-6
„Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.“

Amri ya pili inatimiza na kukamilisha Amri ya kwanza. Kwa sababu hiyo taratibu kadhaa za maelezo ya Agano la Kale zinataja mistari hii kuwa sehemu ya Amri ya kwanza. Hata hivyo, waelezaji wengine wanaoitaja kuwa Amri ya pili wanaiona kuwa amri ngumu na kuleta hali ya kutokufahamu sawasawa.


04.1 - Zuio la sanamu za kikristo

Waislamu na Wayahudi wanashitaki ujumla wa Wakristo kwamba wanavunja amri za Aliye Juu. Wanatushitaki hivi: „Ni ninyi mnaovunja amri kuu ya Mungu. Mnachora picha za aina mbalimbali ya Mwenyezi, na mnawaonyesha watu mambo ambayo akili zenu zisizo sawa zimetengeneza.“ Kuieleza na kuitumia amri hii ilivyo sawa imetokeza migongano mikubwa hata kati ya madhehebu ya kikristo. Washiriki wa makanisa fulani waliwahi kuingilia makanisa mengine na kuchoma vitu vyao vitakatifu. Twatakiwa kutambua kwamba, Mungu katika utukufu wake hawezi kuchorwa. Picha yoyote ya Mungu inamchokoza na kutukana enzi yake tukufu. Picha za watakatifu na wa malaika mara nyingi ni ubatili. Mungu ni mkuu zaidi na takatifu zaidi na mwenye enzi zaidi ya yote tuwezayo kuwaza na kutambua. Yeye ni tofauti kabisa na yote ambayo mwanadamu angeweza kutambua au hata kuchora. Tamko hilo linamjumlisha hata mstadi kama Michelangelo !

Mungu hujifunua mwenyewe kwa watu katika njia mbili kwenye Biblia. Kwanza ajifunua kwa njia ya NENO analotamka kwa wasikilizaji, na pili kwa njia ya maono kwa mwonaji au nabii. Kwenye Agano la Kale Bwana ajifunua mara nyingi zaidi kwa neno lake lenye nguvu, na mara chache kwa namna ya maono. Lakini wakati Mwana wa Mungu alipopata kubadilishwa sura ndani ya utukufu wake wa awali mbele ya Mitume wake, wao walianguka kifudifudi kama wafu, kwa sababu utukufu kuu ulifunua na kuhukumu uchafu wao. Yeyote aliyewahi kuona maono hakuweza kueleza kikamilifu yale aliyoyaona. Waliweza kuyaeleza tu katika mifano.


04.2 - Kuzuia Ibada za Sanamu na Mifano

Tunapochunguza vizuri hiyo Amri ya pili, twaweza kuona kwamba haikatazi kufanya picha ya Mungu. Bali inatuonya kuabudu aina yoyote ya sanamu. Wale wanaoheshimu au kuabudu miungu mingine, sanamu zilizoinuliwa au zilizochongwa kwa mawe au miti, hao ndiyo wa kutazamia ghadhabu ya Mungu.

Sanamu kubwa zilizochongwa zilisimamishwa kwenye vilele vya milima kwenye nchi za Mashariki ya Kati enzi za Agano la Kale. Mara nyingi zilikuwa za mawe na kutumika kwa ibada za hadhara. Pia zilikuwepo za mbao, za shaba au dhahabu zilizowekwa manyumbani na kuabudiwa. Lakini yeyote asiyeamini ndani ya Mungu aliye pekee na wa kweli, anamfungulia mlango atoke maishani mwake, na ndipo roho wachafu huingia upesi. Wayunani enzi za Yesu waliinama mbele za miungu yao, ili wajifurahishe katika tamaa za kimwili. Kabla ya hapo, Wamisri, Wassyria na Wababeli waliwahi kufanya yayo hayo. Kwa sababu hiyo Musa na Manabii walifanya vita kali dhidi ya ibada ya sanamu. Siku hizi twaweza kuzitazama sanamu hizo zilizolaaniwa na manabii zamani; zinaonyeshwa kwenye nyumba za maonyesho ya mambo ya kale hapo Kairo, Bagdad na Beirut. Sasa zimekuwa mambo ya kushangaza watalii, ambao viatu vyao vinakwisha kwa kupanda na kutelemka mara nyingi ngazi za Akropoli kule Athene na za makaburi ya wafalme, tena zaidi kuliko viatu vya hao Wayunani na Wamisri wa zamani. Watu hujaribu kufanya yasioonekana yaonekane, na huku hawaridhiki na mahubiri ya Neno la Mungu. Mwanadamu hutamani kuona zaidi kuliko kusikiliza.Basi yasioonekana na yasiyoweza kuguswa inabaki kuwa geni kwao. Hii ni sababu mojawapo kwamba, TV ni majaribu kubwa kwa watu wanaotaka kutii Amri ya pili hata hivyo.


04.3 - Sanamu zinazokatazwa na Wayahudi na Waislamu

TV, Video na magazeti zinatumika kwa haraka na kupokelewa kwa furaha katika ulimwengu wa Waislamu, mbali na marufuku kuhusu sanamu tangu miaka 1,350 iliyopita.

Marufuku huo juu ya picha yoyote ilitokeza namna ya sanaa ya pambo ya kiarabu, ambayo inaonekana kote katika utamaduni ya kiislamu Arabuni, kwenye Muskiti, pia kule Uchina na kwenye ngome nchini Moroko, pia na Afrika Kusini. Matokeo ya Amri ya pili kwa Waislamu yanaweza kuonekana pia kwenye michoro yao ya maua na bustani kwa namna ya umbo la mistari (geometrical), ikiwa kwenye karatasi, mbao, shaba au kwa mawe. Hasa mikeka ya nchi za Mashariki ya Kati zenye picha nzuri za kushangaza, zikionyesha bustani au kubuni habari ya paradiso, hizo zimetambuliwa sana kwa uzuri wake ulimwenguni kote.

Waislamu kule Arabuni lazima watumie mchoro wa mtu bila kichwa, ili kuonyesha mtu akitembea kwa kutaka kuvuka barabara kwenye njia panda. Hata leo ni kinyume cha sheria kuchora kichwa cha mtu. Lakini nchini Iran, Uturki na India, Waislamu hawajisikii kufungwa na sheria hizo, ingawa zimo kwenye Kurani. Hao wanachora hata picha za Mhamadi na malaika Gabrieli, mambo ambayo ni kinyume cha sheria kwa Waislamu wa kiarabu hadi leo.

Hivi karibuni nchi Fulani ya kiarabu ilipotengeneza sinema kumhusu Mhamadi, hawakuruhusu uso wake utokee. Filamu hiyo nzima ilitengenezwa kana kwamba Mhamadi aliona sehemu zote kwa macho yake na kusema kwa sauti yake mwenyewe. Lakini hakutokea wakati wowote nafsi yake mwenyewe. Kwa sababu hiyo, hata watengenezaji wa sinema za kikristo lazima wawe waangalifu wanapokusudia kuonyesha picha za manabii wa Mungu, malaika au Kristo, kwa ajili ya kuwaonyesha Waislamu.

Wayahudi nao wametumia amri yapili kwa uangalifu kwa kujizuia kuchora mfano wa Mungu. Wakati jemadari wa kirumi Tito aliposhinda Yerusalemu mwaka AD 70 na kuingia ndani ya hekalu, hata ndani ya patakatifu pa patakatifu na kutazamia kukuta sanamu ya dhahabu au vyombo vya thamani. Lakini aliudhika kwa kutokupata kitu. Patakatifu pa patakatifu akaikuta tupu, maana Mungu ni roho, wala si wa kushika. Hawezi kuingizwa ndani ya sanduku au kufungwa hata ndani ya mfano au sura ya sanamu.


04.4 - Je, picha za Kristo ni kinyume cha maandiko?

Wakristo hawafafanui amri ya pili jinsi Wayahudi na Waislamu wanavyofanya. Kristo akawa mwanadamu wakati wa kuzaliwa kwake. Kila jicho liliweza kumwona. Alitamka hivi: „Yeye anionaye mimi amemwona na Baba“ (Yohana 14:9). Shabaha ya uumbaji ulifikiwa ndani ya Kristo. Biblia linatueleza, „Mungu akaumba mtu kwa mfano wake; kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanaume na mwanamke aliwaumba (Mwanzo 1:27). Adamu na Hawa waliamriwa na wawe mawakili wa Mungu. Sura ya mwanadamu inakusudiwa kurudisha (au kuonyesha) utukufu wa Mungu hata leo hivi.

Sisi tunayo mapendeleo ya kufurahia uumbaji wa Mungu na tunaweza kuchora maua yake, wanyama na hata watu wake. Lakini kwa vyovyote tusiwafanye kuwa kimungu au kuwaabudu. Viumbe vyote vinaendelea kuwa viumbe. Haviwezi hata kidogo kufikia usawa wa Mwumbaji mwenyewe na hivyo visingepata kuabudiwa. Mfano wa Mungu ndani ya mwanadamu ulipotoka baada ya kuanguka kwake katika dhambi, wakati uovu ulipoenea kote duniani. Lakini Yesu, Adamu wa pili, alirudisha mfano wa Mungu ndani ya mtu. Hivyo haishangazi kwamba Paulo amwita Jesu kuwa, „ni mfano wa Mungu asiyeonekana“ (Wakolosai 1:15).

Yesu alizaliwa, akafa na kufufuka kwa ajili ya wanadamu wote. Hivyo kila mtu aweza kumchora Yeye jinsi aonavyo mwenyewe, kwa sura yake ya kiafrika, sura ya mashariki, ya kizungu au ya nchi za mashariki ya kati. Yeye ni sura ya Mungu kwa umbo la mtu ndani ya utamaduni zozote. Furaha yake, amani na subira yake hazikuwa za shauri ya akili tu, lakini ya namna ya kutumika kwa busara. Ndani ya Kristo, Mungu alitukaribia kabisa. Hakutokea katika sura ya mtu wa kijeshi wa kuogofya, lakini kama Mwana Kondoo wa Mungu mnyenyekevu, aliyekuwa tayari kujitwisha ghadhabu ya Mungu kwa niaba yetu na kufa kwa ajili ya dhambi zetu, ili sisi tuweze kuishi pamoja naye daima. Tena ametufundisha maana ya sadaka (au dhabihu). Msalaba imekuwa ni ishara ya upendo takatifu. Ufufuo wa Kristo kutoka kaburini ulikamilika katika kutokea kwake, kulichtuonyesha mwili Wake wa kiroho na hata hivyo ya kugusika (Luka 24:39).


04.5 - Sura ya Kristo ndani ya wafuasi wake

Bwana Yesu alikuwa anajaa mioyoni mwa wafuasi wake kwa roho yake ya utulivu, ili kwamba upendo, utakatifu na furaha ya Mungu zijionyeshe ndani yao. Ametuamuru tuwe wa mfano wa Mungu katikati ya ulimwengu uliojaa chuki na kifo. Ametupatia upendeleo kuwa “barua za Kristo” zilizo hai, zikisema kwa njia ya tabia yetu katika familia zetu, katika ujirani wetu na kwa rafiki zetu.. Yesu alitia sura yake mwenyewe ndani yetu, ili nasi tuweze kurudisha sifa zake. Yeyote anapokutana na wafuasi mashuhuli wa Yesu kule Afrika, Asia, Ulaya au Marekani au kokote kule, basi ataweza kutambua nuru ya amani ya Kristo iking’aa katika nyuso zao. Wakati roho wa msulibiwa na mwenye kufufuka, huyu Bwana Yesu inatawala ndani ya moyo wa mtu, awe mtajiri au maskini, msomi au bila kusoma, mzee au kijana, atarudisha mng’ao wa ulimwengu wa mbinguni. Haitoshi kabisa kugawa dunia katika maskini na watajiri, wakapitalisti na wasocialisti; ingefaa zaidi kuwagawa katika wale waliozaliwa mara ya pili na wale waliokufa katika dhambi.. Wakati wo wote Kristo anapoona nafasi ya kuishi ndani ya moyo wa mtu, uhai wa Mungu utakuwa wazi ndani yake na utaonekana na watu wote.

Roho Mtakatifu hawerzi kutuongoza ili tujivune sisi wenyewe, lakini anatusaidia kumtukuza Mwana wa Mungu. Tusikubali kuvutwa na uangalifu juu yetu sisi wenyewe kana kwamba sisi ni kituvu cha ulimwengu. Utukufu wo wote unapasa kumwelekea Mwana Kundoo aliyechinjwa kwa ajili yetu. Mariamu, mama wa Yesu, pamoja na watakatifu wote wangekataza kabisa watu kuheshimu sanamu au picha zao. Wangzivunja kote wanakoweza kuziona, kwenye madhabahu, manyumbani au kote hadharani. Hakuna aliyeweza kurudisha utukufu wa Mungu ila Yesu tu. Hakuna mtu aliye mwema isipokuwa ni Mungu tu. Sisi tumekuwa haki na kutakaswa kwa neema Yake tu. Ni kinyume cha Biblia kuomba dua kwa Mariamu au kwa mtakatifu yeyote na kuomba maombezi kwao. Jambo hilo lingkuwa ni kutendea jeuri dhidi ya amri ya pili, kana kwamba kutokumtegemea Baba yetu wa mbinguni, bali kugawa tumaili letu kati yake na viumbe vyake kadhaa walio wa muda nao. Hakuna kabisa mfano, sanamu, kumbukumbu au masalio zinazoweza kutenda mwujiza au kutoa nguvu ya kuponya. Mungu pekee anayetuokoa, tena kwa njia ya Yesu Kristo Mwana wake tu. Sanamu zote, hata ndani ya makanisa ni chukizo machoni pa Bwana.

Ndani ya Agano Jipya tunapata kuonja ushirikiano wa binafsi na Mungu, Baba yetu kama watoto wake wapendwa. Upendeleo huo unahakikishwa kwa njia ya kifo cha Yesu kinachotulipia dhambi zetu na maombezi yake ya kudumu ya kikuhani akiwa mkononi mwa kulia kwa Babaye. Mwana ametengeneza uhusiano wa moja kwa moja kati yetu na Baba yake. Yeyote asiyetumia njia hii, basi haamini ndani ya Ubaba wa Mungu. Tumepokea neema, haki na msamaha, pia na uhai kutoka kwa Baba tu na Mwana wake kwa njia ya Roho yake Mtakatifu. Kwa sababu hiyo inatupasa kushukuru Utatu wa Mungu tu, tena kwa moyo wetu wote.


04.6 - Juhudi ya Mungu

Ufa mkubwa unaokaa katikati ya watu wanaompenda Mungu na wale wanaoelekea mbali naye unaweza kuonekana katika utofauti wa tisho la malipo na ahadi ya baraka katika tamko la amri ya pili. Hapo napo Mungu ajieleza mwenyewe kuwa “Mimi”, linaloonyesha kwambaYeye ni nafsi aliye hai pamoja na makusudi na uwezowa kusema. Anasisitiza kwamba yeye ndiye Bwana mwaminifu asiyebadilika na kutawala mambo yote. Amejifungamanisha nasi katika agano la milele na huku anatazamia hayo nayo toka kwetu kwa kujitoa kwake kabisa na kwa uaminifu.

Mungu hudai upendo wetu. Anakataa kushiriki kujitoa kwetu kwa jambo lolote lingine kama sanamu, mwanzilishi wa dini Fulani, mfalme, au hata dhahabu na shaba. Yeye ndiye Mungu pekee, wala hakuna Mwokozi mwingine.


04.7 - Wale wanaomchukia Mungu wataanguka

Ole wao wanaodharau upendo wa Mungu au kuuchukua kwa juu juu tu! Wao wanafanana na tawi lililokatwa na zabibu. Watakauka na kuchakaa, na kuelekea kwao ni moto wa milele. Tunapokataa kudumu ndani ya Mungu, aliye asili yetu, tunatenda maasi ya kiroho, kwa sababu tunatoa nafasi kwa roho za kigeni, sanamu au nguvu zilizo chafu, au hayo yatatufanya kuwa nusu mungu. Mungu hata shiriki utukufu wake na yeyote ila Mwana wake na Roho yake. Hakuna kabisa Mwumbaji mwingine. Yeye pekee ndiye Hakimu juu ya muda wetu na hata umilele.

Ikiwa mtu hamgeukii Mungu wa kweli, lakini kuchungulia kwa miungu mingine au kwa kujiangalia mwenyewe kana kwamba yeye ni kiini cha yote, atakuwa na kiburi na kufanya moyo wake kuwa mgumu kwa upendo wa Mwumbaji wake. Mtu wa namna hii atakuwa mjeuri na mwovu. Atatumia wengine kwa faida yake badala ya kuwahudumia. Mtu asiyempenda Mungu hataweza kumpenda jirani yake pia. Hawezi kufahamu ulimwengu wala mahangaiko yake ya kiroho kwa sababu anapungukiwa na vipimo vilivyo sawa. Kutokana na hayo, dhamiri yake itakuwa dhaifu, tabia zake zitaendelea kudhoofika. Mwishowe atakuwa anapotoka na mbaya kuliko mnyama katika shughuli zake za ukatili, ili aweze kushinda.

Basi Mungu anawaacha hao waanguke wanaonang’ania kutengana na Yeye, baada ya Yeye kuwaonya na mara nyingi kuwaonyesha upendo wake. Mwisho awatoa kwa tama za mioyo yao, hata wajiangamize wenyewe. Mfalme Sauli pia na Yuda Iskariote ni mifano ya kwanza kwa matokeo kama hayo. Mpango huo tukufu wa hukumu hutendeka kwa mtu mmoja mmoja sawa na kwa taifa nzima. Hata wanaume au wanawake wa ndoa husukumwa kufanya mabaya na wenzao, na matokeo yake, hata maisha ya watoto wao yanapata matatizo.

Hii ndiyo jinsi ya kutokuamini itakavyorithiwa toka kizazi hata vizazi. Familia inayotawaliwa na uchoyo au wivu itaonyesha hali hiyo katika mazingira na tabia yake. Au kama mazingira ya familia inaathiriwa na ubinadamu wa juu juu au ya kuishi bila Mungu kisocialisti, basi matokeo ni yale yale. Roho ya familia inajionyesha ndani ya macho ya watoto.Familia kadhaa zimeshughulishwa na uaguzi, uramali au uchawi kwa tegemeo la kupata kupona , au kwa kufunua mambo fulani yaliyofichika. Shughuli zote hizozimelaaniwa na Yesu, na hata hivyo hatamtupa nje mtu akiungama. Badala yake, atampokea kwa furaha na kumweka huru na laana ya Shetani. Yesu alisema, “Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli” (Yohana8:36): Mamlaka ya Yesu inavuka kabisa uwezo wetu wa kufahamu. Yeye pekee aweza kuvunja mapingo yyoyote ya kishetani.

Mungu anatufundisha kwamba ugumu wa mioyo katika familia utaadhibiwa hata kizazi cha tatu au cha nne, isipokuwa toba la kweli linatokea na washiriki wa familia wanamgeukia Mungu. Mara nyingi watoto na hata watu wazima ni matokeo ya mnyororo wa mababu walioishi bila Mungu. Hata hivyo, tusije tukawalaani wale walio na moyo wa ufisadi, bali tujaribu kuelewa historia yao ya nyuma na kuwapenda. Kuna Wayahudi na Waislamu waliofundishwa mazoeo ya babu zao zinazomkataa Mwana wa Mungu kabisa kabisa. Wanaishi ndani ya mapingo ya jumla kutenda dhambi na kumkataa Mwokozi wa ulimwengu.

Lakini yeyote atamaniye awe huru na nguvu hizo dhidi ya Ukristo lazima akataae uhusiano yake na watu kama hao na kuachana na vifungu vyote vya utamaduni huo kwa ajili yake Yesu. Hata hivyo, tunapoondoka kwenye ulinzi wa familia zetu na usalama wa nchi ya nyumbani, basi tutapata kuona kwamba Mungu kweli ni Baba yetu. Yeye atachukua wajibu kwa ajili ya maisha yetu ya mbeleni. Yeye hutuhakikishia kwamba, “Mimi ndimi Bwana, Mungu wako, Baba yako wa kukupenda daima. Nakufahamu, nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu; unishike kabisa, na uachane na vifungu viovu na vichafu kabisa. Tegemea ndani ya uaminifu wangu na mamlaka yangu, nawe utakuwa huru na salama milele na milele”.


04.8 - Uneemefu wa baraka kwa wale wampendao Mungu

Kama mtu yeyote akimpenda Mungu na kumheshimu, atasingatia juu ya Neno lake na kuishi kwa nguvu yake. Yeyote akitambua kina cha neema yake kwa ajili yetu, ataendelea kwa shukrani kwa ajili ya kuwekwa huru na subira yake. Tutaonyesha kwa maneno yanayokolea tutathibitisha upendo wetu kwake na kwa kumshukuru kwa moyo wetu wote.

Mwumini mwenye shukrani atagundua hazina, nguvu, baraka na uongozi safi ndani ya Neno la Mungu kila siku. Je, wewe ungewaza nini juu ya bibi arusi, ambaye baada ya kupokea barua ya bwana arusi wake, hataifungua na kusahau kabisa habari yake? Basi tungesema kwamba hampendi mwenzi wake. Kinyume cha hayo, bibi arusi mwaminifu atangojea kwa hamu barua ya mwenzi wake. Na wakati wowote apatapo barua, ataifungua mara na kuisoma tena na tena na kutafakari juu ya matamshi Fulani, ambayo yatachapwa ndani ya kumbukumbu yake bila kufutika. – Tunapompenda Mungu, tutajifunza Neno lake kana kwamba ni barua za mapenzi toka mbinguni zilizoandikwa binafsi kwa ajili yetu. Tutarudia kuzisoma na kukumbuka kimoyo maandishi hayo yenye maana sana kwetu. Mioyo yetu itajaa na Neno la Mungu, maana inatuwezesha kutimiza mapenzi yake.

Kama wazazi wataomba kwa uaminifu kwa ajili ya nyumba zao, watavuta mibaraka ya Yesu juu ya washiriki wote wa familia zao. Watoto wao hawatakua bila Mungu au kwa hali ya kutokujali. Badala yake watakuwa na msingi imara. Kwa kweli, wazazi hawawezi kuwalazimisha watoto wao kumwamini Kristo, wala kuwatakasa na maovu kwa kuwapiga.

Lakini mfano bora wa mzazi mwenye tabia ya upendo itatenda kazi polepole, lakini kwa kina itaingiza mema ndani ya akili yao ya nafsini. Watoto mara nyingi wanakumbuka tabia ya wazazi wao zaidi kuliko hata maneno yao. Jicho la mama mara kwa mara litasema kwa sauti kubwa kuliko maneno yake, na upendo wake unavuka hata ng’ambo ya kaburi.

Mungu awaahidi wale wampendao kwamba, watabarikiwa hata vizazi elfu baada yao! Ahadi hiyo inatoa faraja kuu kwa wazazi, ikiwa wanatakiwa kulea watoto wao katika mazingira yanayojaa majaribu na kutokuamini. Nguvu ya upendo wa Mungu hujiingiza katika giza jinsi mwangaza wa jua unavyotia nuru ndani ya jumba lenye giza. Urithi wa kiroho wa nyumbani utaongezeka mara nyingi, kama wazazi ni waumini wenye kuomba.

Je, umewahi kujaribu kutambua kwa kuhesabu naykati zinazokumbwa na vizazi elfu? Tukiweka miaka 25 kwa muda wa kizazi kimoja, ndipo tutakuta miaka 25,000 ya baraka tele za Mungu, kama matokeo ya mwumini mmoja tu aombaye kwa moyo. Au tikitafakari habari ya wajukuu katika familia kubwa, ndipo tutakuta namba kubwa ya wazao, kama jeshi kubwa la kiroho, ambao wote wao watajikuta wamebarikiwa kwa sababu ya wazazi walioamini na kutii. Mungu huwahakikishia wapenzi wake kwamba, kila mwumini mwaminifu atakuwa kama chemchemi ya upendo kwa ajili ya mamia ya watu. Mfuasi mmoja wa Yesu huwa hadai kwamba, yeye ni chemchemi ya uaminifu mwenyewe, zaidi anajiangalia kuwa kama mfereji wa neema ya Mungu. Kutoka katika ukarimu wake Mungu hutoa neema juu ya neema bila masharti kwa wale wampendao na kumtegemea.

Kama tumetambua matokeo ya baraka ya wazazi wetu wa kimwili na wa kiroho kwenye maisha yetu, basi tutaweza kufahamu uzuri wa manufaa ya utamaduni mbalimbali ulimwenguni. Mahali ambapo Neno la Mungu limeongoza vijiji au miji au makundi ya watu miaka hata mamia ya nyuma, utaona na kusikia matokeo yake. Ambapo watu wamewekwa huru na Yesu, wanatoa shukrani na kusaidiana wao kwa wao. Mungu anapopewa nafasi kuongoza utamaduni fulani kwa njia ya Rohoyake Mtakatifu, ndipo familia, shule, viwanda na siasa zinaguswa zaidi kuliko tunavyoweza kuelewa.

Hali kinyume cha hayo in kweli kwa nchi, ambazo wanaabudu miungu iliyonyunyizwa na damu kama vile India, au wakiabudu roho za wafu kama vile Uchina au Afrika, ambapo kuabudu sanamu na matamshi ya siri zinatazamiwa kuleta usalama. Mashirika ya watu kama hawa wanatawaliwa na hofu, utumwa na mashaka. Mara nyingi tu heshima ya mwanamke inaburutwa matopeni, mwanaume anapotawala juu yake. Vita za kikabila zinazuia maendeleo, na maskini wanazidi kuwa maskini. Unapoingia kijiji cha kiislamu, cha kihindi au cha kikristo, utatambua haraka hali ya hewa ya kiroho wa mahali pale. Hata mifugo husikia kama wanapigwa bila huruma au wanatumiwa kwa uangalifu.


04.9 - Jumlisho: Matengano ya maana

Mibaraka ya wazazi wanaoamini inaonekana katika yale wanayotengeneza kwa mtu mmoja mmoja au kwa familia fulani kama matokeo ya upendo thabiti ya mababu kwa Mungu. Mababu kama hawa waliomba na kuchapa kazi wakiishi maisha ya uaminifu hadi uzeeni mwao. Kwa kweli, kuna mstari wa kutenganisha hao wampendao Mungu na wale wanaomchukia, mstari huu ukipita katikati ya ulimwengu mzima. Ikiwa unamtegemea Mungu kweli kama Baba yako, unatulia ndani yake kama mtoto na kukuza tunda la upendo wake.

Upande wa pili, fulani akijizuia na wito wa Mungu, basi ataenda mbali na utawa. Haishangazi kuona kwamba, upendo wa wengi unafifia katika siku hizi za mwisho. Mtu asiporudi kwa Mungu, basi atakuwa ni chemchemi ya maovu. Mafafanuzi ya kiakili yenye hatari yatajileta kama matokeo ya maasi dhidi ya Mungu. Karl Marx alikuwa ni mwaminifu kwa Mungu katika ujana wake, lakini alipokamatwa na maaguzi na kuingia katika dunia la roho za siri, basi aliwaongoza mamillioni ya watu kwenye upotovu, wakichagua njia ya materialism (kwamba hakuna roho wala ulimwengu usioonekana) kuwa namna yao ya kuishi. Hata hivyo, wafuasi wake hawataweza kujenga paradiso ya wafanya-kazi hapo duniani, hata wakitingisha ngumi zao usoni mwa Mungu. Yeyote atakayemkinahi Mungu, aliye asili ya upendo na uzima, na akitukuza watu kama Mungu badala yake Yeye aliye pekee, basi atafufua uchungu na mashakiki moyoni mwake, na kwa mwenendo huo atavuna ghadhabu ya Mtakatifu siku ya hukumu.

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on August 01, 2017, at 01:59 PM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)