Previous Lesson -- Next Lesson
3. Matazamio ya Paulo katika safari zake (Warumi 15:22-33)
WARUMI 15:22-33
"22 Ndiyo sababu nilizuiwa mara nyingi nisije kwenu. 23 Lakini sasa, kwa kuwa sina wasaa tena pande hizi, tena kwa miaka mingi nimekuwa nikitamani kuja kwenu; 24 wakati wowote nitakaosafiri kwenda Spania [nitakuja kwenu.] Kwa maana natarajia kuwaona ninyi nikiwa katika safari, na kusafirishwa nanyi, baada ya kukaa kwenu kwa muda. 25 Ila sasa ninakwenda Yerusalemu, nikiwahudumia watakatifu; 26 maana imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kutoa mchango kwa ajili ya watakatifu walio maskini huko Yerusalemu. 27 Naam, imewapendeza, tena wamekuwa wadeni wao. Kwa maana ikiwa Mataifa wameyashiriki mambo yao ya roho, imewabidi kuwahudumia kwa mambo yao ya mwili. 28 Basi nikiisha kuimaliza kazi hiyo, na kuwatilia mhuri tunda hilo, nitapitia kwenu, kwenda Spania. 29 Nami najua ya kuwa nikija kwenu nitakuja kwa utimilifu wa baraka ya Kristo. 30 Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; 31 kwamba niokolewe kutoka kwa wale wasioamini katika Yudea, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu; 32 nipate kufika kwenu kwa furaha, kama apendavyo Mungu, nikapate kupumzika pamoja nanyi. 33 Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amina."
Mwanadamu hufikiri na Mungu huongoza. Paulo alisogeza mawazo yake kuhusu safari yake ndani ya moyo wake, akionyesha hamu yake, pia na akiombea. Alikuwa amehubiri katika nchi za magharibi na kaskazini za Bahari ya Kati, ambapo alianzisha makanisa kadhaa, mbali na mateso ya hatari aliyopambana nayo. Sasa basi, alitamani kuhubiri upande wa magharibi ya utawala wa Warumi, pia na kwenye baridi ya kaskazini ya Ulaya, kwa shabaha ya kutiisha ulimwengu wote uliojulikana kwa wakati ule, wawe chini ya miguu ya Mwana wa Mungu.
Paulo alikiri kwamba, alijaribu mara kwa mara kutembelea kanisa la Rumi apate kuimarisha imani yao, upendo na tumaini; lakini kwamba, magumu na uwezekano kule Asia Ndogo na Uyunani yalipinga matazamio yake na kusudi lake la kusafiri.
Miaka iliyotangulia Paulo alikuwa akitaka sana kutembelea Rumi apate kufahamiana na kanisa, ambalo lilikua pale pasipo yeye, na alipenda aliimarishe. Wakati wa safari yake kwenda Spania alikusudia kukata safari kule kwa muda, ili atembelee washiriki mbalimbali wa kanisa pale. Pia alitazamia kwamba, kanisa la Rumi lingetegemeza huduma zake mpya kule Spania, pia na kumsindikiza kwa maombi, matoleo na huduma za kimwili. Na hayo yote kwa kusudi kwamba, kuhubiri kwake hapo mbeleni, kusiwe ni faida yake tu, bali libebwe na watakatifu wa Rumi. Paulo alijiona mwenyewe kushurutishwa asafiri kwanza kwenda Yerusalemu apeleke ile changizo ya makanisa ya Uyunani kwa wale waliokuwa maskini katika kanisa la asili, waliokuwa wameuza mali zao kwa sababu ya imani yao katika kurudi kwake Kristo mapema, na kwa matokeo ya hayo walipata njaa. Alikuwa amewafundisha waumini wa makanisa mapya ya Anatolia na Uyunani, kama matokeo ya maumivu hayo, waendelee kuombea kwa imani na bidii, nao waendelee kushinda katika hayo. Pia aliwafundisha waendeshe pia kazi zao kwa bidii, kwa kusudi kwamba, hali yao ya kumngojea Kristo arudi, kusiwe sababu ya kuondoa au kupunguza namna yao ya kuwa na riziki.
Paulo aliandika kwa kanisa la Wathessalonike kwamba, ikiwa mwanaume fulani hafanyi kazi, basi na asile (2. Wathessalonike 3:10). Hata hivyo, hali ya umaskini ya waumini katika kanisa la Yerusalemu ilidai msaada wao kifedha; na jambo hilo lilikuwa ni thibitisho kwa Paulo kwamba, Wakristo toka kwa Mataifa walikuwa na imani imara, kwa vile walikuwa tayari kutoa sadaka hiyo.
Mtume alisema kwamba, ilipasa kwa makanisa mapya ya watu kutoka kwa Mataifa washirikiane katika kusaidia waumini wa asili ya kiyahudi, kwa vile walipata kushirikiana nao katika utajiri wa kiroho walizojaliwa waumini wa kanisa la mwanzo hapo Yerusalemu, ambao waligawa kwa uhuru kwa mtu yeyote vipawa vile vya kiroho na ufahamu uliofunuliwa kwao.
Kwa sababu hiyo, Paulo aliwaandikia kwamba, wale waliozaliwa kwa upya ndani ya makanisa mapya ya watu wa Mataifa, basi inawapasa kwa adili kusaidia walio maskini kati ya watakatifu kule Yerusalemu kupooza taabu zao za kibinadamu. Kutokana na maneno hayo ya Paulo tunatambua kwamba, msaada kwa wale wasiojiweza ni huduma takatifu na ya lazima, ambayo inawezekana kujionyesha popote na kwa wakati wo wote.
Baada ya kupeleka msaada ule wa fedha hadi Yerusalemu, Paulo alikusudia kusafiri hadi Spania kwa kupitia Rumi, ili apeleke na ukamilifu wa baraka za kiroho za Kristo kwa waumini wa kule Rumi. Hata hivyo alisikia mwenyewe ndani yake kwamba, safari yake kwenda Yerusalemu ilikuwa na tatizo kubwa, maana aliishi kule katika makanisa ya pale, ambayo yalishika sheria za Musa, nao walitazama kwa kunung‘unika jinsi Kristo alivyokusanya waumini kutoka kwa Mataifa.
Basi waumini wa Wayahudi karibu walikuwa tayari kukataa hii michango, kwa sababu ilikuwa imetumwa kutoka kwa watu wasiokuwa Wayahudi. Na saidi ya hapo, Waandishi na Mafarisayo walionyesha waziwazi fujo dhidi ya Paulo, hata wakaamua kumwua. Kwa sababu hizo Paulo aliwataka waumini wa Rumi wamwombee bila kukoma katika Jina lake Yesu kwa ajili ya usalama wake, pia na kumbeba katika vita yake ya kiroho kwa ajili ya ukweli kwamba, ahesabiwa haki kwa neema, wala si kwa sheria. Aliwaita Wayahudi, waliokuwa mbali na Yesu kwamba, hao ni watu wasioamini na wanaokusudia kumhukumu na kumwua. Mbali na ufahamu wake wa hiyo tatizo iliyomngojea kule Yerusalemu, aliendelea kulikaribia jiji lenye hatari ya kufa kwake; alifanya jinsi Yesu alivyofanya hapo kabla yake. Maana ni hapo ambapo Yesu alitufia, ndipo akafufuka kwa ajili ya kuweza kutujalia haki; huo udhaifu wa Kristo ukapata kuwa ushindi wake.
Paulo alijumlisha mipango na matazamio yake akisema kwamba, Mungu akipenda, pengine atawafikia hao waumini wa Rumi kwa furaha. Alifunga waraka wake, huku akiomba kwa Mungu wa amani awe pamoja nao wote, hata kama hawakukubaliana kuhusu vyakula, kutahiriwa na mambo mengine yasiokuwa na uzito zaidi.
SALA: Ee Baba wa mbinguni, imekwisha kuwa pendeleo kwetu kwa njia ya Mwana wako Yesu kukushukuru, kwa sababu mtume Paulo alikazana kabisa kupeleka Injili kwa kila mtu, na alitaka kuvuta Mataifa wote kwako, bali alipelekwa kama mfungwa hadi Rumi kwa uchungu na dharau. Twakushukuru kwa barua zake. maombi, imani na tumaini. Utusaidie, tusije tukazunguka tu kwa mambo ya kwetu, wakati upendo wetu unatuongoza kwako tu.
SWALI:
- Kwa nini kabla ya safari yake kwenda Spania, Paulo alitaka kuelekea Yerusalemu, ingawa alijua habari ya tatizo na hatari nyingi zilizomngojea kule?