Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- Romans - 071 (Problems of the Church of Rome)
This page in: -- Afrikaans -- Arabic -- Armenian -- Azeri -- Bengali -- Bulgarian -- Cebuano -- Chinese -- English -- French -- Georgian -- Greek? -- Hausa -- Hebrew -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Malayalam -- Polish -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish? -- Tamil -- Telugu -- Turkish -- Urdu? -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

WARUMI - BWANA NDIYE HAKI au UADILIFU WETU
Masomo kuhusu Barua ya Paulo kwa Warumi
SEHEMU 3 - HAKI YA MUNGU HUJIONYESHA MAISHANI MWA WAFUASI WA KRISTOS (Warumi 12:1 - 15:13)

8. Masumbufu mahususi ya kanisa la Rumi (Warumi 14:1-12)


WARUMI 14:1-12
1 Yeye aliye dhaifu wa imani, mkaribisheni, lakini msimhukumu mawazo yake. 2 Mtu mmoja anayo imani, anakula vyote; lakini yeye aliye dhaifu hula mboga. 3 Yeye alaye asimdharau huyo asiyekula, wala yeye asiyekula asimhukumu huyo alaye; kwa maana Mungu amemkubali. 4 Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha. 5 Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. 6 Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu. 7 Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. 8 Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. 9 Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia. 10 Lakini wewe je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. 11 Kwa kuwa imeandikwa, Kama niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu; Na kila ulimi utamkiri Mungu. 12 Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu.

Wafuasi wa Kristo wanao maoni tofauti tofauti kuhusu mambo yanayokataliwa na yanayoruhusiwa, maana Yesu hakuweka sheria juu ya hayo; bali alitutolea wokovu kamili, uhakika wa kujaliwa haki, pia na nguvu ya Roho Mtakatifu. Alitumia mipango ya sheria tu kwa ajili ya kushika agizo la kuwapenda watu wote.

Ndiyo sababu tunakuta kauli mbalimbali kati ya kanisa hilo na lingine. Wengine wanaona kula nyama ya nguruwe ni dhambi. Lakini Yesu asema: „Si vinavyoingia mdomoni vinamchafua mtu, bali litokalo mdomoni linamchafua mtu … Maana toka moyoni yanainuka mawazo maovu, uuaji, uzinzi, uasherati, uwizi, maneno ya uongo na kukufuru. Hayo ndiyo mambo yanayomchafua mtu“. Kwa kweli, kula nyama ya nguruwe pengine kutamdhuru mtu kwa kusumbua afya yake, lakini hakutamchafua kiroho.

Baadhi ya Wakristo wanavuta buruma au sigara, wakati wengine wanaona kuvuta ni dhambi ya kufa. Ni kweli, kuvuta kunamdhuru mvutaji kiafya pamoja na wale wa karibu naye, lakini moshi ile mvutaji anayovuta ndani ya mapafu, hiyo siyo roho chafu, bali ni sumu inayoweza kumjeruhi, ambayo bora ajizuie kwa ajili ya afya. Kwa hiyo basi, jambo la kuvuta lenyewe si dhambi, ila avutaye ni mwenye dhambi sawa na wote wengine nao.

Wengine wanakataza vileo na dawa za kulevya, nao wako sawa, kwa sababu anayejihusisha na vinywaji vileo au zile dawa za kulevya atapata kuwa mtumwa wa hayo. Hivyo basi, sisi tunamshauri kila mtu ajizuie kabisa na vileo na dawa za kulevya. Kunywa kiasi kidogo cha kileo kwa ajili ya afya ni sawa. Hata hivyo, inatupasa kusema kwamba, maji safi na nyeupe ndiyo kinywaji bora na yenye afya tunachopewa na Mungu moja kwa moja.

Swali hasa lililoinuka makanisani wakati wa mtume Paulo lilikuwa ni hilo: „Je, ni dhambi kula nyama ambayo imetolewa kuwa sadaka kwa sanamu“? - maana wengine walikula nyama hiyo, wakiwa hasa na hamu kwa hiyo. Wakati wengine waliangalia tendo hilo kuwa chukizo. Paulo alihakikisha kwamba, watu wa namna zote mbili wako sawa, maana nyama iliyotolewa kuwa sadaka kwa sanamu hata hivyo si roho, bali ni nyama. Alitamka hivyo, kwa sababu wengine walifikiri kwamba, nyama hiyo imeshawishiwa na roho za uchafu. Hata hivyo, Bwana Yesu alituunganisha sisi sote ndani ya wokovu wake. Hatumo tena chini ya sheria, bali tumewekwa huru na mambo yasiyo muhimu au ya ujinga.

Jinsi waumini wengine walivyoshika Sabato, wengine Ijumaa na wengine Jumapili, basi Paulo aliwaambia: Ninyi wote mko sawa, maana Yesu hakuweka siku kuwa takatifu, bali watu. Kwa hiyo, mnaweza kusali na kumwabudu Mungu siku yoyote na saa yoyote, maana maombi hayakuwekewa mipaka ya siku fulani, au ya saa fulani, lakini yanawezekana na kufaa kila siku na kwa kila saa.

Ni muhimu sana kwa washiriki wa kanisa kutokudharauliana, au kuhukumiana juu juu, na hasa kwa mambo madogo. Yesu asema: „Msihukumu, ili na ninyi msihukumiwe“. Kwa hiyo, yule aliye imara katika imani asimdharau yule, aliye mdhaifu katika ufahamu, wala asimsumbue katika mwenendo wake, lakini ajizuie kwa njia ya upendo na mazoea kama haya. Inampasa aketi pamoja na wadhaifu, awatie moyo, pia na awasaidie. Na katika tabia ya namna hiyo pia walio wadhaifu wasiwadharau wale walio na nguvu kiimani, wala wasiwasengenye, bali wawapende, kwa sababu Yesu awapenda wote.

Paulo aliwathibitishia watu wote: „hatuwi mali yetu sisi wenyewe, bali tumejikabidhi wenyewe kwake Bwana Yesu kabisa na kwa siku zote. Kwa maana tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tukila au kunywa, tu mali ya Bwana, aliyefanya maisha yake mapya yaishi ndani yetu.“

Jinsi roho ya lawama inajiingiza haraka ndani ya kanisa, Paulo aliwaonya wale wadhaifu na wale wenye nguvu, akiwaambia: Mwe waangalifu, maana wote watasimama mbele ya hakimu wa milele.

Usiwahukumu wengine, bali ujihukumu mwenyewe. Ukiri dhambi zako, tena uyashinde katika jina lake Kristo. Ukifikiri kwamba, inakupasa kuwaweka huru wengine na dhambi zao, sema kwa upole, pamoja na upendo kwa kuimarika katika sala zako; tena ujiangalie sana, ili usijidai kuwa mwenye haki zaidi kuliko wengine. Fanya kila juhudi usije ukawafanya waumini wengine wajikwae kwa sababu ya imani au mwenendo wao.

SALA: Ee Baba wa mbinguni, tunapojipima wenyewe kwenye hali ya utakatifu wako na kwenye ukuu kabisa wa upendo wako, hakuna inayosalia ndani yetu kuhusu heshima, uadilifu au ustahi. Twaomba utusamehe mapungufu yetu, na utusaidie tusiwalaumu wengine. Imarisha upendo wetu, ili tuweze kuwapenda wote sawa, na tujiangalie wenyewe kuwa wa mwisho. Amina.

SWALI:

  1. Je, inatupasa kufikiri au kusema nini, wakati mfuasi mwingine wa Kristo anayo maoni tofauti juu ya mambo mengine ya maisha yaliyo ya namna ya pili (sio muhimu sana)?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on November 17, 2022, at 12:25 PM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)